| Bajeti ya 2011/2012: Kilio cha walimu kimezingatiwa? | Send to a friend |
| Monday, 20 June 2011 21:06 |
| 0digg Na Maisory ChachaKWA miaka mitano mfululizo, sekta ya elimu imeendelea kupewa kipaumbele kwa kutengewa bajeti kubwa.Licha ya ongezeko la bajeti hiyo kwa kila mwaka,bado changamoto katika sekta hiyo ni nyingi hasa upande wa ustawi wa walimu.Matatizo ya walimu yasiyoisha kama vile kulipwa mishahara midogo, mazingira duni ya kufundishia, ukosefu wa mafunzo kazini, ukosefu wa motisha na mengineyo, yamekuwa yakiwavunja moyo walimu. Dhana ya motisha kwa walimu ni pana na kama ingekuwa ikitekelezwa kikamilifu na kwa wakati, bila shaka walimu shuleni wangejituma na kuwasaidia wanafunzi kitaaluma.Vitu kama ujira mzuri, mazingira bora ya kufanyia kazi na kuendelezwa kitaaluma ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuwa motisha tosha kwa walimu. Hata hivyo, kwa muda mrefu vitu hivi vimeendelea kuwa changamoto kubwa kiasi cha kuathiri utendaji wa walimu nchini.Hali hii ni tofauti na ilivyokuwa enzi za serikali ya awamu ya kwanza. Kwa mfano, ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (Unesco)iliyotolewa mwaka 2009, inaitaja Tanzania kuwa nchi ya pili iliyokuwa ikiwalipa walimu vizuri miaka ya 1975, miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki.Ilitanguliwa na Burundi. Lakini kwa mujibu wa ripoti, hadi kufikia mwaka 2004, Tanzania imeporomoka na kuwa nyuma ya majirani zake kama Kenya na Rwanda. Wakati kelele za kuboresha maslahi na hali za walimu zikiendelea, serikali inasisitiza kuwa hakutakuwa na uhaba wa walimu ifikapo mwaka 2015. Napata shida kuamini hili hasa ninapoangalia mazingira yaliyopo. Hivi walimu zaidi ya 10,000 tunaoambiwa watakuwa wakihitimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) pekee, watakubali kufanya kazi katika mazingira duni hasa maeneo ya vijijini? Siamini kufanyika hilo, kwani takwimu za mwaka 2008 kwa mfano zinaonyesha kuwa kati ya wahitimu1,468 wa ualimu ni 905 tu walioripoti kazini. Hata Mkakati wa Maendeleo na Menejimenti ya Ualimu (TDMS) ulioanzishwa na serikali mwaka 2008 wenye lengo la kuboresha maandalizi ya walimu, ustawi wao na maendeleo ya kitaaluma, nao haujaweza kutoa suluhisho. Chapisho la HakiElimu liitwalo “Kurejesha Hadhi ya Mwalimu” linaonyesha dhahiri namna utekelezaji wa program hiyo ulivyogubikwa na siasa. Bajeti inayotengwa kwa ajili TDMS haikidhi matakwa ya utekelezaji wa mpango. Kwa mfano, mwaka 2009 Sh76 bilioni zilitajwa kama kiwango cha chini cha bajeti ya utekelezaji,lakini cha ajabu ni Sh21 bilioni tu zilizotengwa. Mwaka 2010 zilipangwa Sh95 bilioni, zilizotengwa ni Sh50 bilioni. Wakati kiasi kidogo kikitengwa kwenye TDMS, serikali wao waliongeza bajeti ya marupurupu kutoka Sh216 bilioni mwaka 2009/10 hadi Sh 269 bilioni kwa mwaka wa fedha 2010/2011.Nauliza hivi watendaji Serikalini hawajui umuhimu wa motisha kazini? Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu viashiria vya maendeleo Barani Afrika (Africa Development Indicators) ya mwaka 2010, imeweka bayana namna walimu katika nchi nyingi za Afrika, Tanzania ikiwemo wanavyotega kazini. Ripoti inasema utoro wa walimu kwenye vituo vyao ni asilimia 15 mpaka 25, na hata wale walioko vituoni, nusu yao hawafundishi.Uchunguzi wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma (PETS) uliofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwaka jana, unatoa picha hiyo hiyo. Taarifa zinasema asilimia 10 ya walimu wa shule za msingi walio kwenye malipo ya serikali, hawakuwepo shuleni katika kipindi chote cha zoezi hilo lililofanyika Mei mwaka 2008. Wastani wa asilimia 13 ya walimu wa sekondari walikuwa watoro huku katika baadhi ya shule asilimia 70 ya walimu walikuwa hawapatikani. Hasara inayotokana na utoro huo ni Sh11.7 bilioni kwa sekondari na Sh47 bilioni kwa msingi. Ni dhahiri kuwa kukosekana kwa motisha, kunawafanya walimu kutojali madhara ya utoro. Kwa waliopo shuleni, wengi wanalipua majukumu yao kwa kuwa hawana moyo wa kufanya kazi. Serikali ifanye nini? Bajeti ya Serikali katika elimu haina budi kuzingatia uboreshaji wa elimu kwa kusimamia utoaji wa motisha kwa walimu. Na motisha hii isiwe ni ongezeko kubwa la mishahara au marupurupu pekee.Walimu wanaweza kupewa motisha kwa kuandaliwa kufanya kazi katika mazingira bora kama kuishi katika nyumba nzuri na salama na zenye mahitaji muhimu kama vile maji na umeme. Wawe na uhakika wa kuendelezwa kielimu, upatikanaji wa mshahara na marupurupu kwa wakati, upandishwaji madaraja wa kueleweka na madhubuti, kuwapunguzia mzigo wa kufundisha na kuwalipa wakifanya kazi muda wa ziada.Tujifunze pia kutoka Uganda ambao kuanzia mwaka jana wameanza kutoa marupurupu ya asilimia 30 ya mshahara kwa walimu wanaofundisha maeneo yasiyofikika kirahisi. Ni muhimu ongezeko la kila mwaka la bajeti ya elimu kuendana na utatuzi wa changamoto zinazoikabili elimu yetu ili ongezeko hilo lilete tija.Kuongeza wingi wa walimu bila kuweka mikakati madhubuti ya kuwafanya wathamini kazi yao na kuthaminiwa hakutosaidia kumaliza tatizo. Aidha, tusitumie hoja ya ualimu ni wito kwa kushindwa kuwasaidia na kusikiliza vilio vyao. Ni kweli ualimu ni wito ila hoja hiyo isitumike kuwanyima maslahi yao. Ikumbukwe walimu kama wafanyakazi wengine, wanatafuta riziki kwa ajili yao na familia zao. Ni bahati mbaya sana mazingira ya wito huu, hufananishwa na ule wa mapadri. Tusisahau makanisa hupokea sadaka na zawadi ambazo huendesha maisha ya mapadri. Tuwasiliane kupitia; paa@hakielimu.org |
No comments:
Post a Comment