Tuesday, June 21, 2011

Mtikila aishtaki Serikali Mahakama ya Afrika  Send to a friend
Thursday, 16 June 2011 21:20
0digg
Waandishi wetu 
MWENYEKITI wa Chama Cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amefungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, akitaka kusikilizwa na kutolewa uamuzi wa kesi ya mgombea binafsi.

Katika kesi iliyofunguliwa Juni 10 mwaka huu, Mtikila atatetewa na jopo la wanasheria watano wa kimataifa, wakiwamo wanasheria waandamizi wa Umoja wa Mataifa.  Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mtikila aliwataja wanasheria hao kuwa ni Profesa Setondji Adjovi na Thompson wa Shirika la Etudes Vihode la Benin, Profesa Charles Adeogun wa Shirika la Charles Anthony LLP la Nigeria na  Francis Dako wa Benin huku wakisaidiwa na Birdi Njau.

“Wiki ijayo ndio itatolewa tarehe ya lini kesi hii itaanza kusikilizwa,”alisema Mtikila.  Hatua ya Mtikila kufungua tena kesi hiyo inakuja takribani mwaka mmoja tangu jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa, kutoa hukumu iliyokubali rufaa ya Serikali iliyopinga ruhusa ya kuwapo kwa mgombea binafsi nchini.

Juni 17, 2010, majaji saba wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani, walitengua hukumu ya kuruhusu mgombea binafsi iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakisema, suala hilo litaamuliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Mtikila ambaye aliyeenguliwa kugombea Urais katika uchaguzi Mkuu 2010 kutokana na kutotimiza masharti ya kuwa na wadhamini 10,  alisema katika kesi hiyo ya msingi, anapinga vipengele vya Ibara 39, 67 na 77 vya Katiba ya Tanzania na mabadiliko ya mwaka 1992 na Desemba 1994.

 “Mabadiliko haya yalibatilisha Haki ya Ibara ya 21(2) ya Katiba ya nchi, ya kila raia wa nchi yetu kugombea Urais, Ubunge na Udiwani bila kulazimishwa kujiunga na chama cha siasa iliyokuwa imetolewa na Mahakama Kuu, Oktoba 1994,” alisema Mtikila.  Alisema madai mengine ya msingi katika kesi hiyo ni kulinda haki ya msingi ya binadamu ya uhuru wa kujumuika na kuirudishia mahakama uhuru wake na nguvu ya kisheria ya kukosoa makosa ya Bunge na dola.

 Mtikila amefungua kesi hiyo wakati tayari Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wameishtaki Serikali ya Tanzania katika Mahakama  hiyo  iliyopo mkoani Arusha, wakidai kusikilizwa na kutoa uwamuzi wa suala la mgombea binafsi.

TLS na LHRC walidai kuwa suala la kuwapo mgombea binafsi ambalo liliwahi kuzua mjadala na gumzo nchini, ni haki ya msingi ya kikatiba.

Historia ya mgombea binafsi
Oktoba 24 mwaka 1994, Mwenyekiti wa Democratic Party, Mchungaji Christopher Mtikila alishinda kesi dhidi ya Serikali katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ambayo iliruhusu kuwapo kwa wagombea binafsi.

Hata hivyo, baada ya kushinda, Serikali ilifanya marekebisho ya Katiba, badala ya kukata rufaa, ili mgombea binafsi asiwepo nchini.

Mei 5, 2006 jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo, lilitoa hukumu nyingine iliyompa ushindi Mtikila kwa kukubali kuwapo kwa wagombea binafsi, uamuzi ambao Serikali iliupinga kwa kukata rufaa.

 Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Timoth Marko na Furaha Maugo Mwisho 

No comments:

Post a Comment